Simba Sports Club

Simba Queens yaanza na ushindi WPL

28 Oct 2026

Kikosi cha Simba Queens kimeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kilimanjaro Wanderers Queens katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL) uliopigwa Uwanja wa Ushirika Moshi.

Queens ilianza mchezo huo kwa kasi na kuonekana kutaka kufunga bao la mapema lakini ilikosa ufanisi wa kutumia nafasi ilizopata.

Aisha Mnunka alitupatia bao la kwanza dakika ya 20 baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Senaf Demis na kugonga Mwamba.

Senaf Demise alitupatia bao la pili dakika ya 30 kwa mkwaju wa penati baada ya mlinzi wa Kilimanjaro kufanya madhambi ndani ya 18.

Advertisement

Pamoja na kushambuliana kwa zamu lakini dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimazika tukiwa tunaongoza mabao 2-0.

Dakika ya 60 tulipata bao la tatu baada ya mlinzi wa Kilimanjaro kujifunga wakati alifanya jitihada za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Zainah Nandede.

Kocha mkuu, Mussa Hassan Mgosi alifanya mabadiliko ya kuwatoa Fasila Adhiambo, Elizabeth Joseph, Senaf Demis na Asha Omary na kuwaingiza Neema Mtunzi, Elizabeth Nashon, Mabinty Camara na Dotto Evarist.

Baada ya mchezo wa leo kikosi kitasafiri kuelekea jijini Dodoma kwa ajili ya mechi ya pili dhidi ya Fountain Gate Princess utakaopigwa Novemba 4.